Kituo cha runinga cha MTV kinatarajia kumpokonya mwanamuziki kutoka Nigeria, Wizkid tuzo aliyoshinda na kumkabidhi mwanamuziki Ali Kiba kutoka Tanzania baada ya kubainika kuwa mshindi halali wa tuzo hiyo ni Ali Kiba.
Wizkid alitangazwa kushinda tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Afrika iliyotolewa na MTV EMA (MTV Europe Music Awards) wakati wa utoaji tuzo uliofanyika mapema mwezi huu lakini kwenye tovuti ya MTV, mwanamuziki Ali Kiba ndiye alionekana mshindi.
Baada ya hali hiyo kutokea watu wengi kupitia mitandao ya kijamii wameitaka MTV kutolea maelezo suala hilo kwani lilizua sintofahamu miongoni mwa mashabiki wa Ali Kiba.
Akizungumza leo usiku kupitia ukurasa wake wa Facebook, Ali Kiba alisema kuwa baada ya malalamiko mengi ya mashabiki, waandaaji wa tuzo za MTV EMA walimtumia ujumbe kuwa yeye ndiyo mshindi halali na kuwa tuzo hiyo italetwa nchini.
Aidha, Ali Kiba amewashukuru mashabiki wake kwa kuwa naye bega kwa bega na kumpigia kura katika kila tuzo anazoshiriki.
Wanamuziki waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ni Wizkid kutoka nchini Nigeria, Ali Kiba kutoka Tanzania, Back Cofee, Casper Nyovest wote kutoka Afrika Kusini na Olamide kutoka Nigeria.
0 comments:
Post a Comment