Mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya chama cha CUF huenda ukaathiri ushiriki wake kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 27 baada ya pande zote mbili zinazosigana kujiandaa kuteua wagombea.
Mbali ya mgogoro huo kuhofiwa kukiathiri chama pengine hadi kusababisha wagombea wake kuzuiwa, pia unaweza kuudhoofisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Habari kutoka ndani ya chama hicho zinasema upande wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa uko kwenye maandalizi ilhali ule wa Katibu Mkuu, Seif Sharrif Hamad unatarajiwa kukutana na watendaji wa chama kujadili ushiriki wao.
Profesa Lipumba aliyeiongoza CUF tangu mwaka 1995, alijiuzulu kwa hiari uenyekiti wake Agosti 2015 lakini siku chache kabla ya CUF kuitisha mkutano Agosti mwaka huu wa kujadili barua yake, aliandika barua ya kutengua kujiuzulu na akarejea kazini.
Siku ya mkutano mkuu uliofanyika Ubungo Plaza, wajumbe waliridhia kujiuzulu kwake lakini walipoingia kuchagua mrithi wake, wafuasi wa Profesa Lipumba walivamia mkutano na kuuvuruga hali iliyosababisha baadaye kusimamishwa kwake.
Alipoulizwa jana namna CUF yenye mgogoro itakavyoshiriki uchaguzi wa madiwani katika kata 22 Bara na ubunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro alisema wapo katika mikakati kuhakikisha wanashiriki kikamilifu.
Mtatiro alisema muda wowote kuanzia sasa Katibu Mkuu, Maalim Seif atakutana na watendaji wa chama kujadili kwa kina suala hilo na kutoa maelekezo.
“Tutashiriki vizuri na niwaweke wazi Watanzania kuwa shughuli za chama zinaendelea kama kawaida hivyo kamati za utendaji zitatimiza wajibu wake wa kuwapitisha wagombea watakaojitosa kwenye kinyang’anyiro,” alisema.
Kuhusu Profesa Lipumba, Mtatiro alisema, “Hatuwezi kufanya kazi na mtu wa CCM kumsogeza karibu yetu ni kumleta atuharibie chama jambo ambalo hatuwezi kuliruhusu. Ingekuwa lile suala la kujiuzulu aliteleza tungemwelewa na kumsamehe lakini inavyoonekana yupo kwenye mipango yake katu hatuwezi kumuweka karibu.”
Lakini Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF anayemuunga mkono Lipumba, Abdul Kambaya alisema, “Tuna kikao leo (jana) upande wa Bara chini ya Mwenyekiti Profesa Lipumba kujadili suala hilo la uchaguzi, kuhusu upande wa Zanzibar sifahamu chochote.”
Akizungumzia uchaguzi huo mdogo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu alisema Ukawa utakuwa bega kwa bega na CUF katika uchaguzi huo kwani wanaitambua kuwa iko moja si mbili kama inavyotengenezwa na watu wasiopenda maendeleo ya chama hicho.
“Tunatambua na kuheshimu uamuzi wa wanachama na viongozi halali wa chama, CUF iko moja, kama kuna mtu anatengeneza propaganda alifanya hivyo akiamini anakwenda kukiua chama ajue bado kinaendelea kusimama,” alisema.
“Pale atakaposimamishwa mgombea kutoka chama hicho Ukawa tutamuunga mkono na kumpigania kuhakikisha anashinda. Tunaamini pia nao watafanya hivyo akisimamishwa mgombea wa Chadema, ”alisema Mwalimu
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Juju Danda alisema mgogoro wa CUF hautaleta changamoto yoyote kwenye Ukawa kwa kuwa wanamtambua katibu mkuu. Alisema Ukawa unamtambua Maalim Seif na ndiye mtendaji mkuu wa chama hivyo watakuwa tayari kushirikiana naye katika kila jambo.
Kuhusu mpasuko unaoendelea ndani ya chama hicho, Danda alisema suala hilo waachiwe CUF wenyewe ndiyo watakaoamua. “Mtendaji Mkuu wa chama ni katibu si Mwenyekiti, na kwa kuwa tupo pamoja na Maalim hatuoni changamoto yoyote yeye ndiye anayesimamia uteuzi na tunategemea mambo yatakwenda sawa,” alisema.
Katika hatua nyingine hatima ya Jaji Sekieti Kihiyo anayesikilkiza kesi ya CUF kujitoa sasa itajulikana Desemba 14 atakapotoa uamuzi wa maombi ya wadai kumtaka ajiondoe.
Jaji Kihiyo alipanga kutoa uamuzi wa maombi hayo dhidi yake jana baada ya kumaliza kusikiliza hoja za pande zote katika kesi hiyo, ambazo zilizua mvutano mkali baina ya mawakili wa wadai kwa upande mmoja na mawakili wa wadaiwa pamoja na Jaji Kihiyo kwa upande mwingine.
Kesi hiyo imefunguliwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamnini wa CUF, dhidi ya Profesa Lipumba, Naibu Katibu Mkuu wa chana hicho Bara, Magdalena Sakaya pamoja na wanachama wengine tisa waliosimamishwa uanachama wa chama hicho.
Wengine ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ambaye ndiye mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mdaiwa wa pili.
Kesi hiyo ilitarajiwa kusikilizwa jana lakini kabla ya kuendelea, kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, Juma Nassoro aliieleza mahakama kuwa wadai wameandika barua wakimtaka jaji ajiondoe kuendelea na kesi hiyo kwa maelezo hawana imani naye.
0 comments:
Post a Comment