The blog is about hard news



Sunday, December 4, 2016

YUSUPH Manji Atimuliwa Jengo la Quality Plaza. Apewa Saa 24


MAKAMPUNI yaliyo chini ya mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Mehbub Manji, yamepewa saa 24 yawe yameondoka katika jengo la PSPF PLAZA, zamani likijulikana kama Quality Plaza, vinginevyo yatang’olewa kwa nguvu na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart.

Notisi iliyotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma – PSPF ambao ndio wamiliki inataja kampuni zilizoko kwenye jengo hilo katika Kitalu Namba. 189/2 kwenye Barabara ya Nyerere kuwa ni Quality Group Company Limited, Gaming Management Limited, Q Consult Limited, Quality Logistics Company Limited na International Transit Investment Limited, ambazo ziko chini ya Manji.

Uamuzi wa kuyatimua makampuni ya Manji, Diwani wa Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, unafuatia uamuzi wa shauri lililokuwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi ambao ulitolewa na Jaji Mgetta Novemba 24, 2016, ambapo pamoja na mambo mengine, iliamuliwa kampuni hizo ziondoke mara moja.

"Katika shauri husika, Mahakama iliamuru miongoni mwa mambo mengine, kuondoka mara moja kwenye eneo husika linalojulikana kama PSPF Plaza, zamani Quality Plaza, lililoko kwenye Kitalu Namba. 189/2 kwenye Barabara ya Nyerere. Unatakiwa uwe umeondoka kwa amani katika muda wa saa 24 kuanzia tarehe ya notisi hii. Zingatia kwamba, kama hutaondoka katika muda wa saa 24, Mfuko umemwagiza dalali Yono Auction Mart and Co. Ltd kukuhamisha kwa nguvu," imeeleza notisi hiyo ya Desemba 2, 2016 kwenda kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality Group of Companies.

Manji kwa sasa ni mshauri wa makampuni ya Quality Group baada ya kujiuzulu rasmi uenyekiti mnamo Julai 15, 2016.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blogger.

Copyright © JARIDALETU BLOG | Powered by Blogger