Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge
Mstaafu wa Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora Mhe. Samwel Sitta.
Mhe. Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika
hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa
akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na
masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samwel Sitta na kwamba Taifa
limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na
maendeleo.
“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na
tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi
katika ngazi mbalimbali za siasa na Serikali.
“Kupitia kwako Mhe. Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa
Marehemu Mhe. Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo na
familia nzima ya marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Wananchi wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na
msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt. Magufuli amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki
kigumu cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Ameni”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Novemba, 2016
0 comments:
Post a Comment