RAIS Dk. John Magufuli ni yule yule. Ndivyo unavyoweza kumtafsiri kupitia misimamo na kauli zake mbalimbali ambazo amepata kuzitoa kabla na baada ya kupewa dhamana ya kuliongoza Taifa hili.
Kwa uhalisia baadhi ya kauli zake huzaa misimamo thabiti inayobebwa na sheria za nchi. Kwa maana nyingine kauli na misimamo yake husimamia kile anachokiamini kuwa ni ukweli na haki.
Ujumla wa misimamo na kauli zake zimekuwa zikigusa hisia miongoni mwa watu wengi na kusababisha mitazamo chanya na hasi kulingana na mtu mmoja mmoja anavyotafsiri.
Pamoja na hali hiyo, misimamo na kauli zake anazozitoa hajawahi kuyumba hata mara moja.
Kwa watu waliopata kufuatilia aina ya kauli za Rais Dk. Magufuli tangu anaingia kwenye ulingo wa siasa za nchi (enzi akiwa waziri), wanafahamu bayana kwamba siku zote amekuwa ni mtu mwenye kauli za misisitizo na msimamo thabiti.
Mtazamo huo unadhihirisha kwamba tangu awali Dk. Magufuli amejipambanua kuusemea ukweli pasipo kujalisha kama ukweli huo ni mtamu au mchungu kwa wengi.
Historia inaonyesha kwamba, wakati akiwa Waziri wa Ujenzi na Miundombinu chini ya utawala wa awamu ya tatu, aligoma kupelekwa kwa boti mbili za mwendo kasi katika Ziwa Victoria kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwa madai kwamba uzito wa boti hizo unaweza kuvunja madaraja ya barabara zitakazotumiwa kupitishwa kwa boti hizo.
Waziri mwenzake aliyekuwa anahusika na Mawasiliano na Uchukuzi wakati huo, Profesa Mark Mwandosya, alijaribu kuingilia kati suala hilo kwa kutetea kwamba boti hizo ni muhimu kwa usafirishaji ndani ya Ziwa Victoria na hazikuwa na uzito wa kuweza kuharibu madaraja kutokana na takwimu walizokuwa nazo.
Dk. Magufuli kwa upande wake alikataa utetezi huo wa waziri mwenzake kwa kusema: “Kama mnataka zikateni vipande vipande hizo boti mkaziunganishe Mwanza.”
Kwa msingi huo ililazimu boti hizo zipitishwe nchini Kenya kwa kupitia Bandari Kuu ya Mombasa na kubebwa kwa magari hadi Bandari ya Kisumu ndiko zikaweza kuingizwa ndani ya Ziwa Victoria.
Pia, msimamo wake wa kuzuia mabasi marefu (Megabus) ya Zambia yaliyokuwa yanatoka Bandari ya Dar es Salaam nao uliwahi kutikisa diplomasia baina ya Tanzania na nchi hiyo.
Inaelezwa kwamba, Dk. Magufuli aliyazuia mabasi hayo Kibaha mkoani Pwani, akidai kwamba sheria za Tanzania haziruhusu mabasi marefu ya kiwango kile kupita katika barabara za hapa nchini.
Pamoja na kuwapo kwa maelezo kwamba mabasi yatakuwa ‘transit’ bila abiria na hayafikii urefu wa malori kama semitrailers ambazo zinaruhusiwa kupita katika barabara zetu, bado Dk. Magufuli alishikilia msimamo wake kwa kusema: “Wazambia watafute namna nyingine ya kuyapeleka mabasi yao Zambia, si katika barabara zetu hata kama hayana abiria yako transit tu.”
Sakata hilo lilikuwa kubwa sana hadi ikabidi ngazi za juu upande wa Zambia na Tanzania ziingilie kati ndipo mabasi yakaruhusiwa kwenda Zambia.
Tukio la kupandishwa kwa nauli ya Kivuko cha Kigamboni pia ni sehemu ya misimamo ya Dk. Magufuli, alisema: “Nauli mpya lazima zilipwe na mtu asiyetaka ni vyema akapiga mbizi kutoka Kigamboni hadi ng’ambo ya pili au apite Kongowe kuingia katikati ya jiji.” Kauli hiyo iliibua mjadala mpana na kugusa hisia za wengi.
Msimamo huo ambao aliutoa mwishoni mwa mwaka 2011, ulionekana dhahiri kutoungwa mkono na wananchi walio wengi lakini aliusimamia kwa nguvu zake zote.
Kwa mantiki hiyo, misimamo na kauli zake alizopata kuzitoa siku za nyuma wakati akitumikia nafasi za uwaziri ukalinganisha na misimamo na kauli zake za sasa akiwa kwenye nafasi ya ukuu wa nchi ni dhahiri unabaini kuwa Dk. Magufuli ni yule yule aliyezoeleka katika msisitizo na kauli zenye kutafsiriwa kwa utata na baadhi ya watu.
Duru zaidi za mambo zinatanabaisha kwamba, kinachoonekana kuisisimua zaidi jamii katika mtazamo wa hofu juu ya kauli za Dk. Magufuli kwa sasa ni nafasi aliyonayo kwamba anatoa kauli au msimamo kama Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa msisitizo wa kauli au msimamo wake unamaanisha kwamba, ni amri na lazima ifuatwe kwa sababu chini ya mamlaka yake kuna vyombo vinavyolinda utekelezaji wa amri yake.
Mfano mapema mwezi huu wakati alipotembelea wakazi zaidi ya 200 wa Mkoa wa Kagera waliokumbwa na tetemeko la ardhi Septemba mwaka jana, aliwaambia bayana kwamba kila mtu atabeba msalaba wake.
Katika maelezo yake alisema kwa uwazi kuwa Serikali haitamjengea nyumba mtu yeyote aliyeathirika na tetemeko hilo kwa sababu si jukumu lake.
Akaongeza kuwa watu wote ambao nyumba zao ziliharibika wanatakiwa kujenga wenyewe kwa sababu hakuna sehemu yoyote duniani ambako Serikali inabeba jukumu la kuwajengea nyumba waathirika wa maafa kama hayo kwa maana kwamba maafa hayo ni ya asili.
“Kuna nchi kama Japan na Italia zimekuwa zikikumbwa na matetemeko mengi, haijawahi kutokea Serikali yao ikawajengea nyumba upya isipokuwa inarejesha miundombinu ya taasisi za umma kama vituo vya afya, shule na barabara.
“Mwaka jana (mwaka juzi) nilipokuwa naomba kura kwenu, sikuomba tetemeko la ardhi litokee hapa, hili ni jambo ambalo liko nje ya uwezo wangu, tunaomba kila mmoja aweze kutumia msaada uliotolewa ili kurejesha miundombinu ya makazi yenu…Wapo wanasiasa ambao watainuka na kuanza kuwadanganya eti Serikali itawajengea nyumba, hilo halipo kama wanaona wanajiweza wawejengee wenyewe,” alisema.
Akaeleza kushangazwa na kitendo cha baadhi ya wananchi wa Kagera kudai tetemeko limesababisha njaa, alihoji kama mazao yao yakiwamo migomba ilipandwa kwenye nyumba.
Baada ya hapo, akiwa katika eneo la Busisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza, nako alisema: “Ninafahamu wapo wanasiasa wachache ambao wanafikiri mzee bure, kila kitu kikitokea Serikali ifanye, Serikali ninayoiongoza mimi haitatoa kitu, mlinichagua niwaeleze ukweli na mimi nawaeleza ukweli.
“Sasa hivi wakati wa kulima mahindi umebadilika, tusijilazimishe kulima mahindi ambayo yanahitaji mvua nyingi, mvua zinaponyesha tulime na asiyefanya kazi na asile, msije kamwe mkadanganywa na mtu yeyote kwamba patakuwa na chakula cha Serikali, nataka niwaambie hakuna shamba la Serikali.
“Nani anaweza akanionyesha shamba la Serikali, hakuna shamba la Serikali, mlinichagua niwaambie ukweli na ukweli utabaki kuwa ukweli ni lazima tufanye kazi tujipange.”
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, wakati akifungua mkutano wa mashauriano wa Bodi ya Makandarasi, Mei mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli, aliwahi kutoa kauli ambazo pia ziliwashtua watu wengi na kuibua mjadala mkubwa.
Kauli mojawapo ni kwamba kiti chake cha urais hajapewa na mtu yeyote bali kimetoka kwa Mungu, hivyo yupo tayari kutoa sadaka mwili wake kwa ajili ya Watanzania wengi ambao ni masikini.
Katika kuweka kumbukumbu sawa, Rais aliitoa kauli hiyo mwezi mmoja baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kukutana na wafanyabiashara Ikulu jijini Dar es Salaam.
Tofauti na kauli hiyo, Rais Magufuli alikwenda mbali na kuwaambia wafanyabiashara hao kama miongoni mwao yupo aliyemchangia fedha wakati wa kampeni ajitokeze na aliwasisitiza walipe kodi.
Pia, Rais amewahi kutoa kauli nzito kwamba, ni mara kumi akachunge ndege kuliko awe rais halafu anavumilia uozo unaofanyika.
Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ni mmoja wa watu ambao wameguswa na kuipambanua misimamo pamoja na kauli zinazotolewa na Rais Dk. Magufuli.
Licha ya maoni yake mengi kuhusu Rais, hivi karibuni aliandika ujumbe kwenye akaunti ya twitter ya Chadema na kusema: “Rais sio Chief Commander tu, ni Chief Comforter, Rais anatakiwa aongee vizuri ni mfariji mkuu tunapokuwa kwenye majanga”.
Tafsiri ya ujumbe huo wa Lissu inawezekana alilenga kumshauri Rais atoe kauli za matumaini na kuwafariji wenye matatizo kwamba kama kuwaambia ukweli basi usiwe ukweli mchungu.
Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, amewahi kukaririwa mwaka jana na gazeti hili akizungumzia baadhi ya kauli za rais kuwa zinaibua tafsiri ya kutia wasiwasi kwa wananchi na kuwajengea taswira hasi wale wanaomlinda.
Muktadha huo wa mtazamo wa Profesa Baregu ambao ulionyesha ugeni wake juu ya kauli za Dk. Magufuli kabla hajawa rais, ulijikita zaidi kuziangalia kauli chache zenye mrengo wa kutafuta huruma ya wananchi ili apate wigo wa kuwabana baadhi ya Watanzania ambao anahisi hawakubaliani naye.
“Anatakiwa ajue kuwa yeye ndiye Commander in Chief (Amiri Jeshi Mkuu), ana vyombo vyote, hivyo kauli zake zinaweza kuweka msukumo wa kuumiza watu wengi kwa kuwahisi tu,” alisema Profesa Baregu.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana, naye amewahi kuchambua kauli za Rais Dk. Magufuli kuwa zinaonyesha udhati wa kupambana na vitendo vya rushwa.
Profesa Bana alisema kwa nafasi aliyonayo Rais kama mkuu wa nchi, anatoa kauli hizo kwa dhamira ya dhati kuwaambia wananchi kwamba hawezi kurudi nyuma katika vita.
Alisema Rais anatumia kauli za aina hiyo ili kufikisha ujumbe kwa wale wanaosema jitihada zake anazozifanya katika utawala wake ni nguvu ya soda.
“Anajua hatari zilizopo ndio maana anasema yuko tayari kujitoa mhanga, si mara ya kwanza tunaona viongozi wa aina yake ambao wamejitoa muhanga kutafuta haki ya wengi wanahujumiwa, lakini pia najua ajenda hii itamvusha 2020 na hilo sitoona ajabu kama ataendelea na mapambano hayo maana najua Watanzania watamuunga mkono,” alisema Profesa Bana.
0 comments:
Post a Comment